Tuesday, 20 December 2016

ZIARA YA MKUU WA MKOA WILAYANI SONGWE KUANZIA TAREHE 18/12 - 19/12/2016

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akiongea na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe katika Ukumbi wa Kanisa la Roman Catholic Kapalala Songwe





Afisa Utumishi Polycapy akitoa taarifa jinsi anavyoongoza na kuboresha Idara ya Utumishi


Mkuu wa Mkoa wa Songwe akiwa na Wakuu wa Idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe aliwasisitiza Watumishi wa Serikali kuwatumikika wananchi kwa kuwafuata katika maeneo yao wala si kuwasubiri wafuatwe maofisini mwao.
Alisisitiza kuwa muda mwingi utumike kuwatumikia Wanyonge wananchi katika maeneo yao.
Alisema Maafisa Mapato watafute Masoko na kubuni vyanzo vya mapato badala ya kukaa maofisini na kushughulikia leseni.
aliagiza kuwa Wataalam wahakikishe wanakuwa na mpango mkakati wa kuwaongezea kipato wananchi.
Chiku Gallawa alisisitiza swala la uwajibikaji na Wataalam kuwa na takwimu zilizo sahihi.
Aidha kuhusu umuhimu wa takwimu Mkuu wa Mkoa alisema Mkoa kwa kushirikiana na Wataalam wa Takwimu wa Taifa wapo katika hatua za mwisho ili kubaini takwimu sahihi za kiuchumi za Mkoa kuanzia ngazi ya kaya mpaka Mkoa mzima.
Hatimaye alisema mkoa unaendelea na mkakati wa kupima kila kipande cha ardhi cha Mkoa wa Songwe ili kupanga matumizi ya ardhi na urasimishaji ili kuepukana na migogoro ya ardhi na kutoa fursa za uwekezaji katika maeneo yatakayotengwa.

Alisisitiza matumizi ya vipimo vya kilo kwa ajili ya kuuzia mazao, alisema hayo wakati akisikiliza malalamiko kutoka kwa wakulima wa Karanga ambao walisema wafanya biashara wananunua kwa kutumia madebe na kupangiwa bei.
Mkuu wa Mkoa alisema wakulima walime aina moja ya zao ili kulima kwa wingi kwa kuzingatia ushauri wa Wataalam kutoka Halmashauri. Alisema kuwa Halmashauri itatafuta mbegu na soko la uhakika. Vilevile alisisitiza matumizi ya mbolea ili kuzalisha mazao kwa tija.

DARAJA LA BARABARA YA KAPALALA - GUA








Chiku Gallawa alitembelea daraja la lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Kapalala - Gua katika daraja hilo Mkuu wa Mkoa aliona sehemu iliyochomwa na raia wasio wema na kuangalia uharibifu uliojitokeza.
Mkuu wa mkoa alitoa agizo kuwa Kata ifuatilie ili kujua ni nani alifanya uhalifu huo na kuhakikisha hatua za kisheria zinachukua mkondo wake.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya alisema kuwa daraja hilo limepangiwa fedha za kufanyia marekebisho katika msimu wa fedha wa 2016/17. Na aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa daraja hilo linalindwa na kutumika ipasavyo Halmashauri imejipanga kununua mzani ili kupima kila gari litakalokuwa linataka kuvuka hapo na kuruhusu uzito unaoruhusiwa tu.

MGOGORO WA WAKULIMA NA WAGUGAJI KAPALALA

Mkulima Joseph Samson aliyevunjwa mkono na Wafugaji akitoa malalamiko kwa Mkuu wa Mkoa


Mfugaji Mayunga Ganji akitoa utetezi upande wa Wafugaji

Mkuu wa Mkoa  alipokea malalamiko  kuhusu mgogoro wa Wakulima na Wafugaji wa kijiji cha Kapalala na akamwagiza Mkuu wa Wilaya na kamati ya ulinzi na usalama kufuatilia swala hilo na kumpatia majibu haraka. Aliongeza kuwa ikibainika mtu akibainika kafaya makosa ya makusudi achukuliwe  hatua za kisheria inayostahili.

       MKUTANO WA KIJIJI GUA





Katika mkutano wa kijiji uliofanyika katika kijiji cha Gua Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa alisikiliza kero za Wananchi na kuzitolea ufafanuzi kwa kutumia Wataalam husika na hatimaye alihitimisha mwenyewe.
Chiku Gallawa aliwaambia wananchi kuwa lengo la ziara ni kuona hali halisi ya Songwe ilivyo ili kujua nini kifanyike.
Kuhusu ombi la kumegewa eneo kutoka mbuga za Wanyama alisema swala hilo linahitaji mchakato mrefu ila mkoa umejipanga kuandaa  mpango wa matumizi bora ya ardhi na urasimishaji ardhi kuanzia ngazi za vijiji. 
Alifafanua kuwa ufugaji wa kuhama hama utakwisha vinginevyo wafugaji wauze  baadhi ya ng’ombe ili wapate eneo sahihi.
Kuhusu huduma za Afya  hususan  kusua sua kwa ujenzi wa jengo la Wodi ya wanawake na Watoto Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mganga Mkuu Msaidizi wa Wilaya abaki kijijini hapo mpaka jengo litakapokamilika.
Kuhusu kutokuwepo shuleni  kwa mwalimu wa shule ya msingi ya Gua kwa muda wa mwezi mmoja kwa sababu ya kuhudhuria mafunzo,  Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya amrudishe Mratibu Elimu wa Kata  kufundisha.
Kuhusu shule ya Sekondari aliwaagiza wananchi wajipange kujenga shule  hiyo na Afisa Elimu wa Wilaya ahamie Kapalala chini ya usimamizi wa karibu wa Mkuu wa Wilaya  na Mkurugenzi pia taarifa ya  maendeleo ya ujenzi ipelekwe kwa Mkuu wa Mkoa kila Mwezi.
Kuhusu kero ya Malipo ya Tumbaku ambayo inahusisha madeni makubwa ya chama cha Ushirika cha Songambele Mkuu wa Wilaya alisema madeni hayo yanahusisha mkopo kwa  baadhi ya viongozi na wakulima, alisema kamati ya ufuatiliaji imeundwa na itaanza kufanya kazi muda si mrefu.
Aidha Mkuu wa Mkoa alisema tume hiyo ianze mara moja na taarifa iwasilishwe kwake mara baada ya zoezi hilo kukamilika.
Aliongeza kuwa tatizo la Barabara, Mkuu wa Mkoa alisema muda si mrefu mkoa utakuwa na huduma za Tanroad ambazo zitasaidia kupunguza kero hiyo.
Kuhusu Mawasiliano ya simu Mkuu wa Mkoa alisema  ataongea na makampuni ya simu.
Mkuu wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa kuvuna maji kutoka kwenye paa za nyumba zao wakati serikali inatafuta namna ya kusaidia miradi mikubwa na aliwaagiza wataalam kuhakikisha elimu ya kutosha inatolewa kwa wananchi jinsi ya kutega na kuhifanyi maji katika njia bora na salama.
Pia alishauri wanachi kubadili mwelekeo wa kilimo cha Tumbaku na kutafuta zao mbadala lenye kuleta tija kwa sababu kilimo cha Tumbaku siyo endelevu kwani siyo rafiki na mazingira.

 MKUTANO NA ZOEZI LA KUCHOMA NYAVU HARAMU MKWAJUNI








Mkuu wa Mkoa alisimamia zoezi la kuchoma nyavu haramu zenye thamani za Tzs 58,000,000.00 aliwashukuru kamati ya ulinzi na usalama kwa kazi waliyoifanya na aliwataka wananchi kufanya uvuvi ulio endelevu na aliwaasa wananchi kuendelea kulinda Ziwa ili liweze kunufaisha kizazi hiki na kijacho.
Alisema uvuvi huu uwasaidie kupata protini kwa afya na madhara makubwa yatakuwa kwa akina mama na Watoto.
Aidha alisema wengine wanatumia mabomu ambayo yanaleta madhara kwa afya ya binadamu.
Chiku Gallawa aliwambia wananchi kuwa Mkoa utazinduliwa mwezi wa Pili hivyo wananchi wajiandae kuuutangaza ili Watanzania wote wajue Mkoa wa Songwe ni kati ya mikoa iliyo bora  Tanzania.
Aliongeza kuwa wilaya ya Songwe ina fursa za kutosha kama  Misitu kwa ajili ya kufuga nyuki, Migodi ya Dhahabu, Makaa na kiwanda cha kuzalisha umeme wa megawati 300 hivyo Wananchi, Viongozi washirikiane ili kuandaa vijana ili wasije wakawa wasindikizaji.


No comments:

Post a Comment