Saturday 10 December 2016

ZIARA YA MAFUNZO KUHUSU EPRS BAGAMOYO

ZIARA YA MAFUNZO YA UKUSANYAJI TAKWIMU ZA WAKAZI BAGAMOYO TAREHE 11  HADI 13 DISEMBA, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akipokelewa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bagamoyo



Mkuu wa Mkoa akipata maelekezo kutoka kwa mratibu wa mradi  wa Ukusanyaji Takwimu za Wakazi kwa njia ya Elektroniki e-PRS Chumi Makurunge Joel kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, na kulia kwa Mkuu wa Mkoa ni Katibu  Tawala wa Wilaya Erica Yagella

Msafara wa ziara ukielekea kwa walengwa ili kuona zoezi la ukusanyaji wa Takwimu katika kata ya Dunda, Bagamoyo






Mkoa na wataalam kutoka Songwe wakishiriki katika zoezi la ukusanyaji Takwimu za Wakazi

Msimamizi mkuu wa mradi wa EPRS na Mkuu wa Chuo cha Takwimu cha Dar es Salaam Prof. Innocent Ngalinda akitoa maelezo kuhusu  utekelezaji wa zoezi la ukusanyaji Takwimu za Wakazi.


Chiku Gallawa akitoa maelezo kuhusu madhumuni ya ziara yake Bagamoyo katika ukumbi wa Mkuu wa Wilaya. 

 Mkuu wa Mkoa alieleza kuwa Mkoa wa Songwe unataka kujifunzo ukusanyaji wa Takwimu za Wakazi kwa sababu umeona ni muhimu kuendesha shughui za maendeleo kwa njia ya kielekroniki kwa sababu kama takwimu zitaandaliwa kwa umakini zitasaidia kufanya shughuli zilizotarajiwa kwa ufanisi mkubwa, urahisi, na gharama ndogo. alitoa mfano kuwa Mkoa wa Songwe upo katika utekelezaji wa mkakati wa kuwapatia Waheshimiwa Madiwani Ipad kwa ajili ya mawasiliano kwa sababu itaokoa muda, Shajala na gharama za usambazaji wa taarifa,


SIKU YA PILI YA ZIARA KATIKA KATA YA MAKURUNGE

lengo la ziara hiyo ilikuwa kupata uzoefu wa changamoto katika zoezi zima la utoaji elimu na ukusaji wa taarifa katika ngazi ya jamii.



Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe Eliya M. Ntandu akieleza viongozi wa kata ya Makurunge kuhusu kusudi la ziara hiyo


Mmoja wa Watendaji wa vijiji akitoa uzoefu wake kuhusu ukusanyaji wa taarifa.             

Katika uzoefu wake Juma alisema baada ya kuanzisha mfumo huo hana kazi tena ya kutafuta taarifa kama alivyokuwa akifanya zamani kwani kwa sasa kila kitu kipo kiganjani. aliongeza kuwa taarifa za mikutano zinafanyika kwa kutumia ujumbe wa simu tu badala ya kugharimia matangazo kwa njia ya magari .



Wengine walichangia kuwa changamoto zipo kidogo kama uhiari kwa baadhi ya watu wachache lakini kama Elimu ikitolewa vizuri faida ni nyingi zaidi ya mapungufu.



TAARIFA YA ZIARA NA MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA ZIARA YA MAFUNZO KUHUSU MFUMO WA e-PRS
1.0 Utangulizi
Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika (EASTC) wamekubaliana kuandaa mfumo ePRS unaotumia simu za mkononi kuchukua taarifa za wakazi kwa kila kaya katika kijiji/mitaa au kitongoji (Sheria ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 1982, Sheria ya Takwimu 2015 na Sheria ya Usalama wa Taifa).
Kwa sasa zoezi la kuandikisha wakazi limeanza katika wilaya ya Bagamoyo mkoa wa Pwani ambako viongozi wa mkoa wa Songwe pamoja  na baadhi ya wataalam, walifanya ziara ya mafunzo kuanzia tarehe 9-13/12/2016 kwa lengo la kupata uelewa mpana wa namna mfumo huu unavyofanya kazi na manufaa yake kwa watunga sera, viongozi wanaofanya maamuzi katika ngazi mbalimbali, kupanga miradi ya maendeleo na ya kijamii.
Mkoa wa Songwe umepanga kusimamia na kuratibu zoezi la usajili wa watu kwa kutumia mfumo mpya wa kieletroniki uliohuishwa, baada ya rejesta ya wakazi kushindwa kutoa matokea yaliyotarajiwa.
2.0 Lengo la Ziara
·      Kufahamu asili na misingi ya kuwepo kwa mfumo wa ePRS,
·      Kupanua ufahamu wa jinsi mfumo unavyofanya kazi,
·      Kuona mafanikio ya zoezi la ePRS,
·      Kujifunza kutokana na changamoto walizokutana nazo na jinsi walivyokabili changamoto, na Kuandaaa mpango wa Utekelezaji wa kuingiza mfumo wa ePRS mkoani Songwe.

3.0 Taarifa ya Ziara
Katika ziara hiyo ya mafunzo iliyohusisha, Viongozi wakuu 2 wa Mkoa, Waandamizi 4, na wataalam 4 walianza safari tarehe 9/12/2016 kuelekea Bagamoyo Mkoa wa Pwani. Katika safari hii kulikuwa na magari na Madereva 3. Wajumbe wote walifika salama na kupokelewa na wenyeji, ambao ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo pamoja, EASTC na UNICEF. Utambulisho ulifanyika kati ya saa 4  na saa 5 asubuhi katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo. Ratiba ya mafunzo ilikuwa kama ifuatavyo:
3.1 Siku ya Kwanza: Kutembelea maeneo yanayoendelea na uandikishaji wa kaya na wanakaya.
Timu ya mkoa wa Songwe iligawanywa katika makundi matano na kufuatana na Wajumbe wa serikali za Mitaa pamoja na “enumerators” wenye simu na GPS. Timu zilipangiwa maeneo ya kata Nianjema, Dunda na Mgomeni.
Mambo ya kujifunza
1.    Namna ya kuingiza taarifa za kaya (mahali ilipo, idadi ya wanakaya, Umiliki wa nyumba)
2.    Kuingiza taarifa za wanakaya kwa kuanzia na Mkuu wa kaya (Majina ya Mwanakaya, Umri, Ulemavu, Jinsi, elimu, picha, Kitambulisho, umiliki wa simu)
Baada ya kutembelea mitaa na vitongoji kuona zoezi la uandikishaji linavyofanyika, na baadhi ya wataalam kushiriki katika uandikishaji kwa vitendo, timu zote tano zilirejea katika ofisi ya mkuu wa wilaya kwa ajili ya majadiliano.
Mkuu wa Chuo cha Takwimu cha Mashariki mwa Afrika aliongoza majadiliano kwa kujibu maswali na changamoto zilizoonekana wakati wa kutembelea maeneo na kujifunza jinsi uandikishaji unavyofanyika. Pia wajumbe waliweza kuona kwa kifupi taarifa zinazopatikana kwenye mfumo wa ePRS.
3.2 Siku ya pili: Kutembelea kata iliyofanikiwa na kukamilisha zoezi la uandikishaji.
Timu ya mkoa wa Songwe kwa pamoja ilisafiri hadi kata ya Makurunge kando ya barabara ya Bagamoyo – Msata, Njia panda ya kwenda Hifadhi ya Saadani.
Msafara uliongozwa na kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Bagamoyo hadi katika ofisi ya Afisa Mtendaji wa kata, ambapo msafala ulipokelewa na Wenyeviti 5 wa Vitongoji  vya kata ya Makurunge.
Baada ya utambulisho, kila mwenyekiti wa kitongoji alisimama na kuelezea jinsi walivyofanikiwa kukamilisha zoezi, manufaa wanayopata na jinsi wananvyoendelea kuuhuisha na kuutumia mfumo. Na baadaye walijibu maswali toka kwa wajumbe.
Mafanikio:

·      Ushirikishwaji wa wajumbe wa kitongoji,
·      Uhamasishaji,
·      Usimamizi,
·      Uwazi,
·      Uwajibikaji na
·      Uzalendo.

Manufaa
·      Kupunguza gharama za matangazo inapotokea jambo la wananchi wote (Kipaza Sauti),
·      Kurahisisha mawasiliano kwa kutuma ujumbe mmoja kwa wananchi katika kitongoji,
·      Kuokoa muda wa wananchi wa kupanga foleni na kusubiri kuandikishwa kwenye Daftari (Zamani),
·      Kupunguza gharama za Shajala,
·      Kuondoa mrundikano nyaraka ofisini,
·      Usalama na upatikanaji wa taarifa,
·      Utambuzi wa wakazi wote katika kijiji, kitongoji, kaya na
·      Kujua idadi, shule na umri wa watoto wote waliopo na wasio kuwepo shule.
Changamoto
·      Baadhi ya Wananchi kutojua umuhimu wa kujiandikisha kwa sababu za itikadi za siasa na dini.
3.3 Siku ya tatu: Kuchambua taarifa muhimu zinazopatikana kwenye Mfumo na mpango kazi wa baadaye
Katika siku hii, kulikuwa na darasa muhimu sana kwa wajumbe. Mkuu wa Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika Prof. Ngalinda alifanya muhadhara wa kina juu ya uchambuzi wa taarifa mbalimbali zinazopatikana kwenye mfumo wa ePRS. Taarifa hizo zinahusu:
·      Idadi ya kaya zote, orodha ya wanakaya, kaya zilizosajiliwa, mkuu wa kaya hayupo, taarifa za elimu, taarifa za elimu kwa eneo, Elimu kwa Umri (Waliopo shuleni), elimu kwa umri (hawapo shuleni), miaka 0-13 (Hawapo shuleni), miaka 5-13 (hawapo shuleni), nyumba za kupanga, idadi ya kaya (Mkuu wa kaya), Cheti cha kuzaliwa, kadi ya mpiga kura, nk
·      Kuandaa mpango kazi kwa ajili mkoa wa Songwe kwa kipindi cha Disemba, 2016 na Januari, 2017 kama unavyoonekana kwenye jedwali na. 1 hapa chini.

Maazimio ya pamoja kati ya Viongozi wa Mkoa wa Songwe, EASTC, NBS na UNICEF juu ya uhuwishaji wa mfumo wa ePRS katika mkoa wa Songwe na Mpango kazi  kwa ajili ya utekelezaji wa Maazimio Desemba 2016-Januari, 2017
Na
Azimio
Walengwa
Muda wa utekelezaji
Mtekelezaji
1
Viongozi wa wilaya ya Bagamoyo kuja mkoani Songwe kufanya ziara ya Uhamasishaji
Viongozi wa wilaya zote za mkoa wa Songwe na wajumbe wa RCC, Afisa Tarafa, DAS, KUU (Mkoa na Wilaya)
Tarehe 21-23 Des. 2016
RAS, NBS, na EASTC
2
Kuendesha mafunzo kwa siku 2 juu ya ukusanyaji wa takwimu za kaya katika wilaya za Mkoa wa Songwe
WEOs 94, MEOs 71, VEOs 307, Watakwimu wa H/shauri 5, ITs 5,    Mtakwimu wa Mkoa 1, RSM 1,
Tarehe 27-28 Des. 2016
Timu za Uratibu za Wilaya, Mkoa na Tarafa
3
Kufanya mikutano ya uhamasishaji (Advocacy Meetings) katika kata 94 na vijiji 307
Afisa Tarafa, Viongozi wa Dini, CSOs, Watu Mashuhuri, Madiwani, Wabunge na Wananchi
Tarehe 3-11 Jan. 2017
RAS, NBS, EASTC, UNICEF
4
Ukusanyaji wa takwimu ngazi ya kaya katika wilaya ya Mbozi kwa siku 20.
WEOs, VEOs, Wajumbe wa Serikali za Mitaa/Vitongoji/Vijiji, timu ya uratibu mkoa na wilaya, EASTC, NBS na UNICEF
Tarehe 12-31/1/2017
1. WEOs, VEOs na wanafunzi 150 watashiriki, Timu ya uratibu Mkoa na wilaya, NBS, EAST na UNICEF

Imeandaliwa na Ofisi ya Mipango na Uratibu - Songwe

No comments:

Post a Comment