Tuesday, 4 October 2016

MKUU WA MKOA WA SONGWE CHIKU GALLAWA AKUTANA NA WADAU WA ELIMU KATIKA WILAYA YA MBOZI

 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameongea na Wadau wa Elimu katika Wilaya ya Mbozi tarehe 04 Oktoba, 2016 katika ukumbi shule ya Sekondari ya Vwawa iliyopo Mbozi, Songwe


Mkuu wa Mkoa akiongea na Wadau wa Elimu




Wakati akifungua kikao kazi hicho, Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa alisisitiza kuwa Sekta ya elimu ni muhimu katika maendeleo ya nchi na itafanikiwa iwapo Wasimamizi watatumia ubunifu wao wakishirikisha wadau mbalimbali ili kutimiza mipango yao waliyojiwekea. 


Mkuu wa Mkoa aliwaasa Waalimu kutimiza wajibu wao " Timiza wajibu wako katika wakati sahihi" alisema.  aliongea hayo akiwataka kuhakikisha wanasimamia tabia njema kwa wanafunzi, kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata ujauzito na utoro mashuleni.  Chiku Gallawa alikemea tabia ya baadhi ya Waalimu wanaoshiriki kuharibu maisha ya Wanafunzi kwa kuwapa mimba. " Mwalimu atakaye bainika kumpa mimba mwanafunzi atafungwa Jela miaka 30" alisisitiza.

Aidha Mkuu wa Mkoa alizungumzia wajibu wa kurekebisha mabadiliko ya tabia nchi kwa kuanzisha vitalu vya miche ya miti 2000 kwa kila shule ambapo, kiasi cha miche itapandwa katika eneo la Kijiji au Mtaa kama itakavyojadiliwa pamoja na Serikali ya eneo hilo, katika maeneo ya shule na miti mingine wanafunzi watapewa ili wakapande majumbani kwao.  

Taasisi za shule na Halmashauri za vijiji/Mitaa ziliagizwa kuhakikisha zinatoa chakula kwa wanafunzi, na aliongeza kuwa  wanafunzi washirikishwe kulima mashamba kitaalam ili  wajifunze mbinu za kilimo bora wakati huo wakipata chakula wakiwa shuleni ili kupunguza tatizo la udumavu wa akili.

Hatimaye alitumia nafasi hiyo kuwataka Wadau kuendelea kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa kuwaelimisha wananchi kuacha kulima kando kando ya mito na kwenye vyanzo vya maji. " Wananchi watii sheria zilizoweka kutokulima kandokando ya mito na kwenye vyanzo vya maji" alikazia.

Mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa kila shule ipange mkakati wa kuvuna maji ya mvua ili kuepuka uhaba wa maji unaoendelea kuwa sugu katika maeneo mengi ya mkoa wa Songwe.

Pamoja na hayo Waalimu walishauriwa kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za kuongeza kipato  bila kuathiri utendaji wao wa kazi ili waweze kuwa mfano katika maeneo yao ya kazi. aliongeza kuwa Waalimu wasiridhike na elimu walizo nazo bali wasome elimu mbalimbali kwa kutumia hata fursa ya umeme unaoendelea kusambazwa katika vijiji na Teknolojia ya Habari na Mawasilano  kwani kuna masomo aina mbalimbali kupitia mitandao. 




No comments:

Post a Comment