Friday, 5 August 2016

Ziara ya Waziri wa Ujennzi, Uchukuzi na Mawasilano Prof. Makame Mbalawa Mkoani Songwe. 



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbalawa amesema hakubaliani na hali ya ujenzi wa jengo la kupokelea wageni katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa Songwe na hivyo kuahidi kufanya uchunguzi ili kujiridhisha na thamani halisi ya fedha iliyotumika na taratibu za kumpata mkandarasi aliyejenga.

Kauli hiyo aliitoa jana katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Songwe alipofanya ziara ya siku moja kuwa hajaridhika na hali ya jingo lilivyo licha ya serikali kutoa fedha nyingi huku jingo hilo likiwa halijakamilika na mkandarasi hayupo katika eneo la kazi kwa muda mrefu.

Alisema  miundombunu ya ujenzi wa majengo katika uwanja huo hakubaliani nayo wakati uwanja ukiwa umejengwa vizuri na kuwa serikali ipo kwenye mkakati wa kuhakikisha ujenzi unakamilika na ndege kubwa zikiwemo za mizigo zianze kutua ili kusaidia kusafirisha mizigo ya wakulima na hivyo kuinua uchumi wao.

“Tumejenga vizuri barabara ya kurukia ndege lakini tunashangaa hatua ua jingo hilo hairidhishi na siko tayari kulipokea hadi hapo nitakapojiridhisha” alisema Mbalawa
Alisema kufuatia hali hiyo serikali itaunda timu ya kufuatilia namna mkandarasi huyo alivyopatikana, thamani halisi ya fedha ikijiridhisha ndipo itakapotoa fedha za kumalizia ujenzi huo ili huduma ziendelee.

Waziri huyo alisema kwa kuzingatia umuhimu wa miundombinu ya mawasiliano sasa serikali ya awamu ya tano imeamua kuwasaidia wananchi ambao wanapata shida kwa kutenga asilimia 46 ya bajeti ya mwaka 2016 hadi 2017 ambayo ni sawa ni zaidi ya Sh. 1.2 tilioni zikiwa zimetengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa  miundombinu.

Kwa upande wake meneja wa uwanja wa Songwe Hamisi Amiri alisema mkandarasi wa kwanza ambaye ni kampuni ya Kundasighn aliacha kuendelea na ujenzi hali ambayo imesababisha kutokukamilika kwa wakati.

Alisema kwa sasa kuna kampuni nyingine ya Shamphrey ambao wameanza kujenga miundombinu ya majengo ambapo hadi sasa mkandarasi huyo hajalipwa kiasi chochote cha pesa hali inayosababisha kzi ya ujenzi kuendelea kusuasua.

Stephano Simbeye, Mwananchi
simbeyesjmwananchi@gmail.com
Watumishi ngazi ya Mkoa na Halmashauri wakimsikiliza Waziri.

 Ziara ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba Mkoani Songwe

Mkuu wa Mkoa Chiku Gallawa akitoa ufafanuzi kuhusu hali ya pembejeo kwa Waziri.

Hali ya afya ya udogo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inadaiwa kuzidiwa na tindikali nyingi, hivyo kuwa chanzo cha kushuka kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali na hivyo kuwakosesha tija wakulima.

Hayo yameelezwa jana na wadau na watafiti katika shamba la Mbegu la Mbozi lililopo eneo la Magamba mkoani Songwe kwa Waziri wa Kilimo, mifugo na uvuvi Dkt. Charles Tizeba kuwa hali ya udongo imekuwa kikwazo kutokana na kuwa licha ya kutumia mbolea za chumvi chumvi lakini hazitoi matokeo mazuri kwa mkulima.

Robert Hamisi ni mtaalamu wa uzalishaji mbegu kutoka Kampuni ya Meru alisema kuwa katika eneo la hekta 220, uzalishaji ulikuwa tani 2.5 hali iliyofanya washituke na kuomba ushauri kwa Kampuni ya Yara ambao walifika shambani hapo na kuchukua sampuli ya udongo na kwenda kupima maabara nchini Norway.

Alisema baada ya kupata majibu ya kipimo cha udongo walishauriwa aina ya mbolea ya kutumia ili kurejesha afya ya udungo inayoongeza virutubisho vilivyopotea na sasa mwaka huu mavuno yameongezeka na kwamba wamelipa hekta 310 wanatarajia kuvuna tani 1320 ikiwa ni ongezeko kubwa.

Akizungumzia suala la afya ya Udongo Waziri wa kilimo, mifugo na Uvuvi Dkt. Charles Tizeba kujua hali ya udongo ni jambo la muhimu ili kuwafanya wakulima wasiendelee na kilimo cha kubahatisha na kuahidi kufanya kila jitihada ili kusaidia sekta ya kilimo.

Alisema alizungumza na wataalamu wa udongo kutoka kituo cha utafiti Uyole ambao wamemweleza kuwa ardhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini inakabiliwa na udongo kuwa na tindikali nyingi hivyo kufanya mbolea za chumvichumvi kutokuwa na tija, hata hivyo alisema wanaweza kutumia chokaa kupunguza hali hiyo.

Hata hivyo alisema kutokana na kuwa katika mkoa wa Songwe madini hayo ya chokaa yanapatikana kwa wingi wataalamu watafika kukagua kama ndiyo yanayofaa kwa ajili ya kupunguza tindikali hiyo ya udongo ili wakulima waweze kuitumia kutibu udongo.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Galawa akizungumza katika kituo cha uzalishaji Mbegu Magamba alikitaka kituo hicho kuongeza ubunifu ili kuweza kuwezesha wakulima wadogo wadogo kujifunza mbinu mbalimbali za uzalishaji wa mbegu na elimu nyingine ili kueneza teknolojia ambayo itasaidia kupunguza tatizo la kuuziwa mbegu bandia.

Alisema wakulima wa mkoa wa Songwe wana uwezo mkubwa wa kulima lakini wanakwamishwa na changamoto ambazo hata hivyo zikisimamiwa vizuri zinaweza kutatulika na kuwa kitendo cha mbegu kusafirishwa kwenda kusindikwa Mbeya kinahamisha ajira za wakazi wa eneo hilo na ni kinyme cha mkakati wa mkoa kuanzisha viwanda ili malighafi zinazozalishwa ziweze kusindikwa katika eneo husika.

Awali katika taarifa yake Mkurugenzi Mtendaji kiongozi wa Wakala wa Mbegu za Kilimo Firmin Mizambwa pamoja na kuwa afya ya udongo kuwa tatizo linalopunguza ufanisi wa uzalishaji lakini pia wakala huo unakabiliwa na changamoto nyingine ikiwemo ukosefu wa umeme wa grid ya taifa ambao unasababisha mbegu zinazozalishwa hapo kusafirishwa hadi Mbeya kwa ajili ya kusindikwa hali ambayo inaongeza gaharama.

Mizambwa aliongeza kuwa pia wanakabiliwa na tatizo la wananchi kuvamia shamba na uharibifu wa misitu ikiwa ni pamja na mifugo kuingia kiholela kwenye shamba.

Stephano Simbeye, Mwananchi
simbeyesjmwananchi@gmail.com

Waziri akipata maelezo ya uzalishaji miche bora ya Kahawa kutoka kwa Mtafiti Mkufunzi Charles Mwingira katika kituo cha Utafiti wa Kahawa TACRI Mbozi.
Waziri Dkt. Charles Tizeba akitoa uzoefu wake kuhusu zao la Kahawa

No comments:

Post a Comment