Mkuu wa
Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akifungua kikao cha Wadau wa Elimu Mkoa wa Songwe
kwenye ukumbi wa sekondari ya Vwawa tarehe 13 February, 2017.
|
Pistory
Mashiku mdau wa elimu kutoka Ileje akisoma maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho.
Wadau wa Elimu toka wilya ya Ileje wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Songwe.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ileje Haji Mnasi akitoa taarifa ya
Halmashauri yake.
WADAU WA ELIMU WAJITWISHA JUKUMU LA
KUUKWAMUA MKOA WA SONGWE KITAALUMA
Na:Daniel
Mwambene,Songwe
Katika kuukwamua mkoa wa Songwe kwenye aibu ya kushika
nafasi ya mwisho tena kitaifa katika matokeo yajayo ya Mtihani wa Kumaliza
Elimu ya Msingi 2017 na kuinua kiwango cha Elimu ya Sekondari wadau wamegawana
majukumu na kuahidi kushika nafasi za juu kitaifa.
Mkakati huo ulifikiwa kwenye kikao cha Wadau wa Elimu wa
Mkoa wa Songwe kilichofanyika katika ukumbi wa sekondari ya Vwawa kikiongozwa
na viongozi wa mkoa huo ukihusisha Wakuu wa Wilaya,Makatibu Tawala,Wakurugenzi
Watendaji Maafisa Elimu, baadhi Maafisa Elimu Kata,walimu wa sekondari na Asasi
zisizo za kiserikali.
Wadau wengine ni walimu ambao shule zao zilifanya vizuri na
zilizofanya vibaya na kusababisha mkoa kuwa wa mwisho kutoka halmashauri zote tano za mkoa huo ambazo ni Songwe,Momba,
Ileje,Mbozi, na Tunduma Mji.
Akifungua kikao hicho,Mkuu wa Mkoa huo Chiku Gallawa aliwataka viongozi wa ngazi mbalimbali kuacha mtindo wa kukaa
ofisini badala yake wawafuate wananchi katika maeneo yao hali itakayowapunguzia
wananchi gharama za kuwafuata viongozi ambao serikali imewapatia vyombo vya
usafiri.
Alisema kuwa,viongozi wa serikali hawana budi kujenga
utamaduni wa kuwatumikia wananchi ili kupokea kero zao pamoja na kujionea hali
halisi kuliko kusubiri taarifa za mezani.
Mh.Gallawa aliongeza,kuwa kiongozi yeyote atakayeonekana kuwa
kikwazo cha maendeleo kwa wananchi kamwe serikali ya mkoa wake haitamvumilia.
Baadhi ya mikakati iliyowekwa ni pamoja na taarifa za Wathibiti
Ubora wa Elimu kufanyiwa kazi na kila mlengwa,uboreshaji wa mazingira ya
shule,upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni,jamii kuelimishwa ili
kuondokana na imani za kishirikina kujenga nidhamu kwa wanafunzi,kuthibiti
utoro wa walimu na wanafunzi.
Mambo mengine ni kutafuta walimu wa mbadala kwenye masomo
yasiyo na walimu,mgawanyo mzuri wa walimu na kutumia njia shirikishi na
fikirishi katika kujifunza na utoaji wa motisha chanya kwa wanafunzi na wadau
wa elimu mkoani humo watakaofanya vizuri.
Ikumbukwe kuwa mkoa huo wenye umri wa miezi takribani kumi
tangu kuanzishwa kwake katika Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi mkoa huo
ulishika nafasi ya mwisho kwa mikoa yote ya Tanzania Bara.
Kabla ya kufikia hatua ya kupanga mikakati hiyo kila
halmashauri ilitoa taarifa yake iliyotokana na vikao vya wadau kutoka ngazi za
wilaya ambayo pia ilitokana na mikakati ya ngazi za kata ukiwa ni utekelezaji
wa maagizo ya Mkuu wa Mkoa huo aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka jana wakati wa
kutolewa kwa matokeo ya Darasa la Saba 2016.
Akifunga kikao hicho Katibu Tawala wa Mkoa huo Eliya
Ntandu alizitaka halmashauri zote kwenda kutekeleza maazimio hayo kwa kuwa na
mpango kazi unaotekelezeka na kupimika.
Ntandu alisema kuwa kila mkakati uliopangwa utafuatiliwa
na kila kiongozi kwenye eneo husika la utekelezaji na atakayelelega hatua kali
zitachukuliwa dhidi yake.
No comments:
Post a Comment